Falsafa za kutajirika kwenye ujasiriamali
Mafanikio katika maisha siyo jambo jepesi ambalo linaweza kuja kimiujiza. Mara nyingi ni hatua ambayo inaanzia mbali ikiandamana na mipango, juhudi katika utekelezaji na hata kukabili vikwazo mbalimbali.
Mtu mwenye mafanikio madhubuti kimaisha mara nyingi anakuwa amepitia misukosuko mingi katika kufikia hatua hiyo. Ni sawa na methali ya Kiswahili isemayo “Ukimwona nyani mzee, ujue kakwepa mishale mingi.”
Leo hii mtu anayeainishwa katika kundi la kukwepa mishale mingi ni Deogratius Kilawe. Yeye ni mmiliki wa kampuni tatu kubwa ambazo alizibuni na sasa zimeanza kuenea kwa kasi katika nchi kadhaa Afrika.
Alizaliwa Dar es Salaam Novemba 30, 1987. Baba yake, John Stanley Kilawe na mama Leah Thomas Kilawe walikuwa wafanyabiashara; Baba akiwa ni mmiliki wa gereji na mama ni fundi wa kushona nguo.
Mazingira ya wazazi wake kuwa wafanyabiashara, anasema yalimfanya awe anatafakari kila wakati tangu akiwa shuleni na hata alipomaliza ni kwa namna gani angeweza kuendeleza mikoba ya wazazi wake kwa kuwa tajiri mkubwa.
Kazi za ujasiriamali
Katika kipindi cha mwaka 1997 hadi 2000, aliwahi kujihusisha na shughuli za ujasiriamali. Wakati huo akiwa anasoma shule ya msingi.
Alikuwa ananunua karatasi sehemu mbalimbali Jijini Dar es Salaam kwa watu mbalimbali na kuziuza katika viwanda tofauti ili kupata fedha. Anasema kazi hizo hazikuhitaji mtaji mkubwa bali uwe mchapa kazi na makini na watu unaofanya nao kazi.
Kazi hiyo ilimpatia fedha yeye na mama yake ambaye alikuwa mmiliki, fedha hizo zilitumika kujipanua kibiashara na hata kutoa ajira kwa watu wengine ambao aliwapa kazi ya kukusanya karatasi na baadaye anazinunua na kuzisafirisha hadi viwandani.
Alijipanua zaidi kibiashara akawa anaokota chupa za maji zilizotumika. Anaelezea kwamba alikuwa miongoni mwa wafanyabiashara wa kwanza wa kuokota chupa na kuziuza.
Hata hivyo, katika miaka ya 2000, watu wengi walijitokeza kuifanya biashara hiyo ndipo akaamua kuachana nayo.
Katika kusoma kwake, anasema alipata vikwazo vingi vilivyomfanya ajikute anasoma shule tatu tofauti, kidato cha kwanza hadi cha nne na hali kadhalika ikawa hivyo hata kwa kidato cha tano hadi cha sita.
Moja ya mambo ambayo yaliwachanganya walimu, anasema alikuwa ni mtundu sana na alikuwa na akili iliyomuwezesha kufanya vizuri darasani ingawa alikuwa hahudhurii vipindi darasani.
Katika mtihani wa taifa wa kidato cha sita, anasema alifaulu na kuwa mwanafunzi bora aliyonyesha kuwa na kipaji maalumu. Katika somo la jiografia alikuwa mwanafunzi bora kitaifa.
Kutokana na ufaulu huo, mwaka 2007 alichaguliwa kwenda kusoma katika Chuo Kikuu cha Mzumbe. Wakati huo alikuwa pia anaendesha biashara yake ya vifaa vya ofisini. Ingawa alikuwa anapenda kusoma taaluma ya uchumi, alibaini kuwa kusoma siyo jambo la muhimu bali mikakati ile ambayo inaweza kumwelekeza kufikia katika kiwango cha mafanikio kwenye hatua aliyokusudia.
Kwa sababu hiyo, anasema kwa kuwa malengo yake yalikuwa ni kufanya biashara aliona hakuna haja ya kuendelea kusomea mambo ya uchumi. Akaamua kuacha chuo wakati anaingia mwaka wa pili.
Baada ya kuacha chuo alianza kujiunga na klabu mbalimbali za kuelimishwa juu ya mafanikio kimaisha kupitia taasisi kama AIESEC na Achievers Club. Aliona kuwa klabu hizo zingeweza kumfanya awe bora zaidi. Baadaye akawa anajihusisha kwenye mafunzo ya biashara. Katika kufanikisha hilo akawa anahudhuria mikutano mbalimbali ya kibiashara Dar es Salaam na hata nje ya nchi. Wakati huo, anasema maisha yalikuwa magumu, alikuwa anavaa viatu vimetoboka na alikuwa akitembea kwa miguu kutoka Kariakoo hadi nyumbani kwao Karakata, wilayani Ilala.
Kampuni zampandisha chati
Ana kampuni tatu, Mikono Speakers, Excel Management and Outsourcing na WOBUPEDIA inayomiliki chapa zifuatazo; Focus Outdoor, Focus Tanzania. Kampuni hizo zote anasema zinalenga kujitanua na kuenea katika nchi mbalimbali Afrika.
Anasema Kampuni ya Excel inaendesha shughuli zake kwa kutoa mafunzo ya rasilimali watu, kuajiri wafanyakazi kwa niaba ya kampuni, kutoa mafunzo ya namna ya kuendesha biashara na washauri wa mambo ya uwekezaji. Kwa sasa ipo nchi tatu; Tanzania, Kenya na Uganda.
Mikono Speakers inafanya biashara ya mikutano mikubwa duniani na kila mwaka inafanya mikutano zaidi ya nchi sita barani Afrika; Tanzania, Kenya, Uganda, Nigeria, Ghana, Afrika ya Kusini na Rwanda.
Wobupedia inamiliki chapa ya Focus Outdoor kwa ajili ya mabango ya matangazo makubwa barabarani na maeneo ya wazi na ya ndani.
Anasema matangazo hayo yanakuwa na nembo Focus Outdoor na mpaka sasa wanamiliki mabango makubwa zaidi ya 200 jijini Dar es Salaam na lengo lao ni kuwa na zaidi ya mabango 450 mpaka Desemba mwaka 2015.
Anasema anajivunia kuwa na kampuni kubwa ya mabango nchini na mwaka huu na anategemea kutumia zaidi ya Sh4 bilioni kwa uwekezaji wa mabango kwenye mpango huo. Mwakani anatarajia kuanza kuwekeza mikoani.
“|Lengo letu ni kupanua Focus Outdoor kuingia katika nchi ya Kenya na Uganda katika miaka michache ijayo,” anasema Kilawe.
Falsafa za kutajirika
Kilawe anasema ili mtu kutajirika inampasa kufuata kanuni au falsafa kadhaa. Miongoni ni kama zifuatazo:
Mafanikio mazuri ni yale ambayo mtu anakua kidogokidogo. Mtu ambaye amepata fedha nyingi kwa wakati mmoja, lazima ipo siku atarudi nyuma. Maana ile fedha hakuipata kwa hatua zile za kukua.Watu wengi wanapenda kuwa matajiri lakini wanataka kufikia malengo hayo kwa njia ya mkato. Fedha ya namna hiyo haiwezi kumfanya mtu akawa tajiri wa kudumu.
Ukweli ni kwamba watu wengi hawapati maendeleo kwa sababu wanaogopa kuingia kwenye tanuru la moto ili waive na baadaye wawe wamekua vizuri kijasiriamali.
Mafanikio lazima yawe hatua kwa hatua. Lazima uungue na kupitia tanuru la moto ambalo litakuchoma taratibu mpaka utakapokamilika na kuiva kwa ajili ya kuliwa mezani. Watu wengi wanataka fanikiwa lakini wanaogopa kupita kwenye tanuru na hufikiria njia za mkato na wengi huishia maisha ya majuto.
Ndiyo maana watu wengi wanaopata fedha nyingi ghafla huwa hawawezi kudumu nazo kwa muda mrefu. Hutumika katika muda mfupi na baadaye hurejea tena kwenye umaskini.
Mafanikio bila maumivu, wala huwezi kuona raha yake. Ukipita kwa njia ya mkato unafika kileleni lakini ipo siku mfumo unabadilika na anguko lake litakuwa kubwa, matokeo yake huwezi kurudi tena juu. Mtu ambaye amepata mafanikio kwa kukua, hata kama ataanguka kibiashara, anaweza akaibuka tena kwa sababu tayari amejiweka kwenye mfumo. Mafanikio ni ile hali mtu anakua, kivutio kwa wengine.
Mtu aliyekua kibiashara anaweza akafanya ujasiriamali popote kwa sababu kanuni ya mafanikio ni zile zile, mahala popote. Sababu za mtu kufanikiwa ni ile kasi ya ama kuiva (amekua) au kuwa tayari kuwa mfanyabiashara.
Mafanikio yanategemea unajua nini, unafanya nini, una mawazo gani, anaona nini, ni watu gani wanaokuzunguka. Mafanikio ni jambo ambalo liko kisayansi na linaweza kuthibitishwa kisayansi. Wengi wanakimbia Afrika kwenda Ulaya lakini kila siku tunapishana na Wazungu wanakuja Afrika ili kuwekeza. Hii ni kwa sababu Afrika ina fursa nyingi za uwekezaji. Waafrika wanakimbilia Ulaya ambako tayari fursa zimeisha.
Kukimbilia Ulaya ni sawa na kwenda eneo ambalo changamoto zimepatiwa ufumbuzi. Huko hakuna tena fursa bali Afrika ndio eneo lenye changamoto tele. Hii ni ishara kuna fursa nyingi ndio maana watu wenye suluhu humiminika Afrika kila mara na ‘kupiga hela ndefu’ (kupata fedha nyingi). Waafrika wanapaswa kuwa makini.
Lengo la biashara ni kutatua changamoto zilizopo eneo fulani. Tanzania ina changamoto nyingi hivyo ina nafasi za fursa nyingi za ujasiriamali. Watakaofanikiwa kutatua suluhu hizi ndio watakuwa na mafanikio.
Comments
Post a Comment